Qurani
/
5- SURAT AL - MAAIDAH /
Introduction
(Imeteremka Madina na aya zake 120) Sura hii ni ya Madina. Idadi ya aya zake ni 120. Sura hii ni kati ya sura za Qurani zilizoshuka mwishoni. Sura hii imekusanya masuala mbalimbali. Miongoni mwa masuala haya ni wajibu wa kutimiza maagano kwa ujumla, ni sawa yakiwa baina ya mja na Mola wake au baina ya watu wenyewe kwa wenyewe. Kadhalika, sura hii imebainisha baadhi ya vyakula vilivyoharamishwa na vilivyo halali, na uhalali wa kuwaoa wanawake wa Mayahudi na Wakristo. Pia sura hii imetaja nguzo za udhu na tayamamu. Kadhalika, imeeleza kutakikana kumfanyia uadilifu adui. Vile vile, sura hii imeashiria Neema za Mwenyezi Mungu juu ya Waislamu na wajibu wa kukihifadhi Kitabu chao. Na ikabainisha kwamba Mayahudi wamebadilisha maneno kutoka mahali pake, na Wakristo wamesahau baadhi ya mambo waliyokumbushwa na kwamba wao wamekufuru kwa kusema kwao kuwa Masihi ni mwana wa Mwenyezi Mungu. Kadhalika, sura hii inayakanusha madai ya Mayahudi na Wakristo kwamba wao ni wana wa Mwenyezi Mungu na vipenzi Vyake. Kisha sura hii imekusanya baadhi ya habari za Mayahudi na kisa cha wana wawili wa Adam. Ni kisa ambacho kinathibitisha kuwa kufanya uadui ni katika maumbile asili ya binadamu. Kisha wajibu wa kuchukua kisasi kwa mwenye kufanya uadui kwa ajili ya kuiweka sawa tabia hii mbovu. Vile vile, sura hii imebainisha adhabu ya kufanya uasherati na kuiba. Tena baadaye, sura hii ikarejea kubainisha ni vipi Mayahudi walivyozipindua hukumu za sheria zilizokuwamo katika Taurati, na ikabainisha kwamba katika Taurati na Injili, ulikuwepo ukweli na haki kabla ya kugeuzwa geuzwa. Pia sura hii imehakikisha kuwa ni lazima kuhukumu kwa mujibu wa Alivyoteremsha Mwenyezi Mungu. Hali kadhalika, imeuashiria uadui wa Mayahudi na Wakristo wa hivi leo kwa Waumini, na kuwalazimisha Waislamu kutowanyenyekea na kutowaridhia kwa wanayowatendea na kuwa ni lazima kuwapinga. Mbali ya hayo, sura imethibitisha ukafiri wa Wakristo waliosema kuwa Mwenyezi Mungu ni mmoja wa watatu! Lakini hata hivyo, Qurani imewasifu baadhi ya Wakristo walioikubali haki na kuiamini. Kisha baada ya hapo, sura hii imemkataza Muumini kujiharamishia mwenyewe vitu vizuri. Na imebainisha kafara ya kuvunja kiapo. Kadhalika, sura hii imeharamisha kabisa ulevi. Na ikabainisha baadhi ya vitendo vya ibada ya hija na cheo cha Kaaba na miezi mitakatifu. Kisha imebainisha upotovu wa baadhi ya mambo waliyojiharamishia Waarabu wenyewe bila ya hoja wala dalili yoyote. Vilevile, sura hii imebainisha hukumu ya wasia wakati wa safari. Mwisho kabisa, sura imehitimishwa kwa kutaja miujiza iliyotokea kwa Nabii Isa (A.S), lakini pamoja na miujiza hiyo, Mayahudi walimkanusha. Pia sura hii imetaja kuwa Nabii Isa (A.S) hana dhambi ya waliopotoka wakamwabudu. Na sura imeeleza Ufalme wa Mwenyezi Mungu Mtukufu juu ya mbingu na ardhi na ukamilifu wa uwezo Wake.
Main Page
Contact us
Links
About us
Site Map