Qurani
/
9- SURAT AT TAWBAH/
Introduction
(Imeteremka Madina na aya zake 129) Sura hii imeteremka Madina mwaka wa tisa Hijria. Ali bin Abi Talib (R.A) aliichukua sura hii kuwapelekea Waislamu katika hija na akawasomea. Kiongozi wa hija hiyo alikuwa ni Abu Bakr Assiddiq (R.A). Aya zake ni 129. Imeanza kwa kujitenga Mwenyezi Mungu Mtukufu na washirikina, na kwa hivyo imeitwa vilevile kama Surat Al Baraa’h, (yaani kujitenga katika dhima, kutokuwa na jukumu). Na baada ya hayo, ikataja utukufu wa miezi mitakatifu na ahadi za washirikina, na wajibu wa kutimiza ahadi nao ikiwa wao hawajaivunja, lakini kama watavunja ahadi, basi yapasa kupigana nao. Na baada ya hayo, sura imebainisha kuwa kiini cha kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ni kumwamini Yeye, na kwamba imani haikamiliki ila akiwa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake wanapendwa na Waumini kuliko kila kitu. Kisha Mwenyezi Mungu Aliyetakasika Akataja kuwa kujiona una nguvu, ndiko kunakopelekea ushindi kuwa mbali Akiiashiria hali ya Waislamu katika vita vya Hunayn. Pia, katika sura hii, washirikina wamepigwa marufuku wasiingie katika Msikiti Mtakatifu wa Makka kwa kuwa wao ni najisi. Na katika sura hii, imetajwa kupasa kuwapiga vita Mayahudi na Wakristo mpaka watoe jizya (kodi) kwa hiari yao nailhali wamenyenyekea. Pia imebainishwa idadi ya miezi mitakatifu. Na humu umebainishwa ulazima wa kutoka kwenda vitani kila vinaponadiwa bila ya kulegalega. Aidha, imeashiriwa hukumu ya wanaobakia nyuma na walemavu wasioweza kwenda kupigana. Kadhalika, imebainishwa hali ya wanafiki ambao wanatafuta fitina kila wakati vinaponadiwa vita. Na Mwenyezi Mungu Akataja namna wanafiki wanavyowatendea Waumini wakati wa amani na wakati wa vita. Katika sura hii, iko amri ya kukata iliyotangazwa kuwatia adabu wanafiki. Nayo ni kuwa Mtume (S.A.W) asimsalie yeyote katika wanafiki akifa. Baada ya hapo, Mwenyezi Mungu Subhana, Ametaja udhuru unaostahiki mtu kubaki nyuma asiende vitani. Na pia Subhana Ameeleza hali ya wale mabedui waliodhihirisha kuingia katika Uislamu, au wakafuata hukumu zake baada ya kuwa Uislamu umepata nguvu. Na Ameeleza kuwa mabedui hao wako kando kando na karibu ya Madina. Na baada ya hayo, Mwenyezi Mungu Ametaja hali za watu kulingana na imani. Akataja pia habari ya msikiti wa udhia walioujenga wanafiki ili upuuzwe msikiti alioujenga Mtume (S.A.W). Kisha Mwenyezi Mungu Subhana Akataja sifa za Waumini walio wakweli katika imani yao na toba ya wale waliobaki nyuma ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W), na Mwenyezi Mungu Akaikubali toba yao. Vilevile, Mwenyezi Mungu Subhana, Ametaja hali za watu katika kuzipokea aya za Qurani zinapoteremka. Mwishowe, Mwenyezi Mungu Subhana Akahitimisha sura hii kwa kusema kuwa hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu Amemteua Muhammad kwa kumpa utume nailhali yeye hataki wapate tabu hao aliotumwa kwao, na kwamba yeye ni mpole na mwenye huruma kwao, na kwamba ikiwa wao watageuka, basi Mwenyezi Mungu Atamtosheleza.
Main Page
Contact us
Links
About us
Site Map