Qurani
/
12- SURAT YUSUF/
Introduction
(Imeteremka Makka na aya zake 111) Sura hii ni ya Makka, na aya zake ni 111. Mwenyezi Mungu Amesimulia ndani yake kisa cha Yusufu katika aya 98 na Ameitangulizia kwa aya tatu Alizotaja ndani yake ufunuo huu Aliomteremshia Muhammad (S.A.W). Ameuita ufunuo huu katika aya ya kwanza “Kitabu kinachobainisha”. Na katika aya ya pili Akauita “Qurani kwa Kiarabu”. Na hii ni kuashiria kwamba ni haki yake uhifadhiwe kwa maandishi na katika vifua vya watu vilevile. Kisha katika aya ya tatu, Akataja kuwa ufunuo huu umekusanya visa vizuri sana, na Akamkumbusha Nabii kuwa hakuwa akivijua kabla ya kuteremshiwa ufunuo. Na hiyo ni dalili kuwa ufunuo huu unatoka kwa Mwenyezi Mungu. Na kisa hiki na sura hii, imemalizikia kwa kutilia mkazo yaliyoanzia. Na Mwenyezi Mungu Akamwelekeza Nabii Wake mnamo aya kumi azingatie kuwa kisa hicho ni katika habari za yaliyofichikana ambazo yeye Nabii (S.A.W) hakuwa akizijua wala kuzijua kweli zake na maelezo yake yalivyo kabla ya kuteremshiwa wahyi. Wala yeye hakuwa pamoja na ndugu zake Yusufu walipokuwa wakipanga mipango yao, na wakiunda njama zao za shari kumuundia ndugu yao kwa baba. Kisha Akamweleza kuwa inadi na husuda huwapelekea watu wengi kuingia katika ukafiri. Na kwamba pupa yake Mtume (S.A.W) kuwa waamini wengi wao haimfalii kitu, lakini kupoza kwake kwa hayo ni kuwa yeye hataki ujira, bali anawaletea Qurani iwe ni uongofu na ukumbusho kwa watu wote. Katika mwisho wa sura, Amewaashiria Mitume ambao Alimtajia visa vyao na misimamo ya watu wao kinyume chao, na vipi mwishowe walivyowashinda makafiri waovu. Na Akasisitiza kuwa ndani ya visa hivi vya Manabii, pana mazingatio kwa wenye akili na kwamba Qurani hii inayovisimulia visa hivi na vinginevyo, si kitu cha kutungwa na kuzuliwa kuwa kinatoka kwa Mwenyezi Mungu kwa uongo bali ni haki na kweli tupu, na ni Kitabu kinachosadikisha Vitabu vilivyotoka mbinguni kabla yake na ni uongofu na rehema kwa watu wanaotafakari, wanaozingatia na wanaoamini. Linaloonekana wazi zaidi katika sifa za sura hii ni kuwa imesimulia kisa cha Yusufu kwa ukamilifu wake. Na kimeonyesha kuwa uhasidi unaenea miongoni mwa watu wa familia moja ikiwa mapenzi wamepewa baadhi yao tu. Kwa hivyo, husuda ya wana wa Yakubu iliwapelekea kumtumbukiza ndugu yao ndani ya kisima kirefu. Lakini Mwenyezi Mungu Alimlinda na vitimbi vyao, kama Alivyomkinga na kishawishi cha mke wa mheshimiwa pale Yusufu alipofikilia utu uzima nyumbani mwa mheshimiwa, na Akamweka vizuri katika nchi ya Misri, na Akamjaalia kuwa nchi hiyo iwe ni makimbilio ya wale waliompangia njama za kumuudhi. Basi hii ndiyo shani Yake Subhana kwa Manabii Wake na vipenzi Vyake. Huwanusuru dhidi ya maadui zao, na Huwathibitisha kwa kuwaweka vyema katika ardhi maadamu wanaishika haki, wanaiamini na wanaishikilia Kamba ya Mwenyezi Mungu.
Main Page
Contact us
Links
About us
Site Map